Mwanamke Mjapani na mwanawe wajeruhiwa katika shambulizi mjini Suzhou nchini China

Basi lililobeba wanafunzi kutoka shule ya Kijapani katika mji wa Suzhou jimboni Jiangsu nchini China lilishambuliwa na mwanaume mmoja anayeaminika kuwa raia wa China jana Jumatatu. Tukio hilo lilisababisha kujeruhiwa kwa raia wawili wa Japani na mwanamke mmoja Mchina yupo katika hali mahututi.

Maafisa katika ubalozi mdogo wa Japani mjini Shanghai wamesema mtu huyo alikuwa na silaha iliyoonekana kuwa kisu. Shambulizi hilo lilitokea wakati basi lililokuwa likiwasafirisha wanafunzi kutoka shuleni lilipowasili katika kituo cha basi.

Mwanamke mmoja Mjapani na mwanawe waliokuwa kwenye kituo hicho walipata majeraha yasiyokuwa tishio kwa maisha. Mhudumu wa basi raia wa China alikuwa katika hali mahututi baada ya kudungwa kisu.

Mtu huyo alipelekwa kizuizini na anafanyiwa uchunguzi na mamlaka.

Kituo hicho cha basi kipo katika eneo la makazi takriban kilomita moja kaskazini ya palipo shule hiyo ya Kijapani.

Ubalozi mdogo wa Japani ulituma maafisa katika eneo hilo ili kukusanya taarifa zaidi.