Moto kwenye kiwanda cha betri za lithiamu nchini Korea Kusini waua 22

Watu ishirini na mbili wamethibitika kufariki kwenye moto uliokikumba kiwanda cha betri za lithiamu karibu na mji wa Seoul nchini Korea Kusini jana Jumatatu.

Wakinukuu taarifa kutoka kwa mashuhuda, maafisa wa idara ya zimamoto walisema moto huo ulianza baada ya seli za betri kulipuka moja baada ya nyingine kwenye kiwanda kilichopo mji wa Hwaseong, jimbo la Gyeonggi. Kulikuwa na takribani betri za lithiamu 35,000 kwenye kiwanda hicho.

Walisema waliokufa ni pamoja na raia wa China 18, wawili wa Korea Kusini na mmoja wa Laos, lakini utaifa wa marehemu mmoja aliyesalia bado haujatambulika.

Miili mingi ya marehemu hao ilikutwa kwenye ghorofa ya pili ya kiwanda hicho, ambapo wafanyakazi walikuwa wanakagua na kufunga bidhaa hizo. Maafisa walisema waathirika walishindwa kujiokoa, pamoja na uwepo wa ngazi zinazoelekea nje.

Rais wa Korea Kusini Yoon Suk-yeol alifanya ziara kwenye kiwanda hicho jana Jumatatu usiku. Alilaumu kutokea vifo hivyo kutokana na uwepo wa nyenzo zinazowaka moto karibu na mlango wa dharura, ambapo alisema ndicho kilichowafanya wafanyakazi waliopo ndani kushindwa kujiokoa. Aliwaamuru maafisa kutathmini chanzo cha ajali hiyo na kuchukua hatua za kuzuia tukio kama hilo kujitokeza tena.