Maswali na Majibu: Tahadhari za mvua kubwa na vidokezo vya kuhama kwa kutumia gari

NHK inajibu maswali kuhusu kukabiliana na majanga. Leo tunakuletea taarifa kuhusu mvua kubwa, mafuriko na maporomoko ya ardhi pamoja na vidokezo mahususi vya tahadhari unapohama kwa kutumia gari.

Usidhani kuwa daima unaweza kuhama kwa usalama ukitumia gari. Wakati wa Kimbunga Hagibis Oktoba 2019, kati ya waathiriwa wote waliofariki nje ya nyumba zao, asilimia 40 walipoteza maisha wakiwa wanakimbia kwa kutumia gari. Baadhi, magari yao yalisombwa. Wengine walifariki baada ya magari yao kuangukia kwenye korongo kando ya barabara.

Wataalam wanashauri watu wasijaribu kwenda nyumbani au kwenda kazini kwa haraka, wakidhani itakuwa salama kwa vile wanatumia magari, hasa ikiwa eneo husika limeathiriwa na mvua kubwa na pepo kali.

Unapaswa kuepuka kuendesha gari kwenye barabara za kando ya mito au mashamba ya mpunga. Mito au mashamba ya mpunga yanapofurika, mpaka kati ya barabara na maji hauonekani. Gari lako linaweza kuangukia kwenye mto au shamba kwa bahati mbaya. Baadhi ya watu wamefariki namna hiyo wakati wa vimbunga na mvua kubwa zilizopita.

Hakikisha barabara unayotumia ni salama ikiwa mvua kubwa imenyesha, hata ikiwa unaijua vizuri barabara hiyo.

Taarifa hii ni sahihi hadi kufikia Juni 24, 2024.