Wazalishaji wa mvinyo kutoka Tottori wavumbua sehemu isiyo ya kawaida ya kuhifadhi bidhaa hiyo ndani ya bwawa

Wazalishaji wa mvinyo katika Mkoa wa Tottori magharibi mwa Japani wamevumbua sehemu isiyo ya kawaida ya kuhifadhi bidhaa hiyo kwenye handaki ndani ya bwawa. Inatoa mazingira sahihi kwa mvinyo wa chupa kuwa bora zaidi katika kipindi kizima cha mwaka.

Handaki linalotumika kwa ajili ya ukaguzi lililopo ndani ya bwawa la Togo katika Mji wa Yurihama limekingwa dhidi ya mwanga wa jua na lina halijoto thabiti ya karibu nyuzi 10 za Selisiasi.

Mazingira ya baridi na giza husaidia kudumisha ubora wa mvinyo mwekundu. Wazalishaji wa ndani wanapanga kuhifadhi mvinyo uliopo kwenye chupa chini ya bwawa hilo kwa hadi kipindi cha miaka mitano.

Mzalishaji wa mvinyo, Sugimoto Satoru alisema: "Mahali hapa ni mazingira mazuri sana kwa mvinyo kuwa bora. Sehemu hii ya kuhifadhia mvinyo inanipa mawazo mengi ya kutengeneza mvinyo wa kuvutia."

Zikiwa tayari kuuzwa, chupa hizo za mvinyo zitawekwa alama kuonyesha zilikuwa zimehifadhiwa kwenye bwawa hilo.