Netanyahu: Mapigano makali ya Israel katika Ukanda wa Gaza yatamalizika hivi karibuni

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anasema Israel iko karibu kumaliza awamu ya mapigano makali dhidi ya Hamas katika Ukanda wa Gaza na itapeleka vikosi zaidi kwenye mpaka wa kaskazini na Lebanon.

Netanyahu alisema hayo jana Jumapili katika mahojiano na kituo kimoja cha televisheni cha Israel.

Alisema haimaanishi kwamba vita vinakaribia kumalizika, lakini vita katika awamu yake kali vinakaribia kumalizika huko Rafah.

Netanyahu alisema kuwa baada ya awamu hiyo kali ya vita kukamilika, kutakuwa na uwezekano wa Israel kuhamishia sehemu ya vikosi vyake kaskazini, na nchi hiyo itafanya hivyo.

Aliongeza kuwa anachukua hatua hiyo kwa madhumuni ya kwanza kabisa kujilinda na pili kuwarudisha wakazi wa Israel nyumbani.

Mapigano yanaendelea kati ya wanajeshi wa Israel na wanamgambo wa Kishia wa Hezbollah wenye makao yake nchini Lebanon karibu na mpaka kati ya nchi hizo mbili. Hezbollah imekuwa ikionyesha mshikamano na Hamas.