Polisi jijini Tokyo watoa onyo kwa kiongozi wa kundi la kisiasa juu ya mabango yasiyohusiana na uchaguzi

Polisi katika Jiji la Tokyo nchini Japani wametoa onyo kwa kiongozi mmoja wa kundi la kisiasa kuhusiana na mabango yasiyofaa ambayo yamewekwa katika ubao wa kampeni za uchaguzi wa ugavana wa Tokyo.

Wachunguzi wameiambia NHK kwamba mabango 24 yenye jina la danguro yamebainika katika ubao wa mabango ya uchaguzi kwenye kata ya Shibuya jijini Tokyo.

Polisi wameripotiwa kutoa onyo kwa kiongozi wa kundi la kisiasa juzi Jumamosi kwa tuhuma za kukiuka sheria.

Kufuatia onyo hilo inaonekana kundi hilo la kisiasa lilibadilisha mabango hayo.

Tukio hilo linafuatia kisa sawia ambapo mabango ya msichana aliye uchi yalionyeshwa kwenye ubao wa kampeni Alhamisi iliyopita, siku ambayo kampeni za uchaguzi wa ugavana zilianza rasmi.

Polisi jijini Tokyo pia walitoa onyo kwa mgombea aliyehusika na mabango hayo kwa kukiuka sheria za jiji hilo.

Wagombea 56, idadi ambayo ni rekodi ya juu, wanawania kinyang’anyiro cha kumchagua kiongozi ajaye wa Tokyo katika uchaguzi wa Julai 7.