Mahujaji wa Kiislam zaidi ya 1,300 wamefariki kutokana na joto kali nchini Saudi Arabia

Waziri wa Afya nchini Saudi Arabia Fahad Al-Jalajel anasema watu zaidi ya 1,300 wamefariki kutokana na joto kali katika ibada ya hija ya kila mwaka.

Kila mwaka, Waislam kutoka duniani kote huzuru maeneo matakatifu ya Makka, magharibi mwa Saudi Arabia.

Mahujaji hutembea mchana na usiku kwa siku kadhaa mjini Makka na maeneo yake jirani.

Mahujaji wapatao milioni 1.8 wameshiriki ibada ya hija ya mwaka huu ambayo imefanyika kuanzia Juni 14 hadi Jumatano wiki iliyopita na halijoto zilipanda hadi zaidi ya nyuzi 50 za Selisiasi.

Kupitia mahojiano ya njia ya simu na kituo kimoja cha runinga nchini Saudi Arabia jana Jumapili, waziri wa afya wa nchi hiyo alisema mahujaji 1,301 wamefariki kwa ugonjwa wa kuzirai kutokana na joto kali na sababu zingine.

Kadhalika Al-Jalajel amesema zaidi ya asilimia 80 ya waliofariki hawakuwa na viza inayohitajika kushiriki ibada ya hija.

Amesema kwamba kushindwa kutumia huduma za usafiri na malazi ipasavyo kunaweza kuwa chanzo cha vifo vyao.