Urusi: Watu wanne wameuawa katika shambulizi la kombora la Ukraine huko Crimea

Mamlaka za Sevastopol zilizowekwa na Urusi katika eneo la kusini mwa Ukraine la Crimea zinasema shambulizi la makombora la Ukraine kwenye mji wa bandari limesababisha vifo vya watu wanne na wengine 144 kujeruhiwa. Urusi inadai kulitwaa eneo la Crimea mwaka 2014.

Wizara ya Ulinzi ya Urusi inasema katika taarifa kwamba shambulio hilo lililotokea jana Jumapili muda mfupi baada ya adhuhuri lilihusisha makombora matano ya ATACMS yaliyotolewa na Marekani kwa Ukraine.

Wizara hiyo inasema vikosi vya ulinzi wa anga vya Urusi vilidungua makombora manne yaliyokuwa na vichwa vyenye mabomu ya kishada lakini kombora la tano lililipuka angani.

Wizara hiyo inasema Marekani inahusika zaidi na shambulio hilo la makusudi la kombora kwa kuwa inaipatia Ukraine silaha. Inaongeza kuwa Ukraine pia inapaswa kulaumiwa kwani makombora hayo yalirushwa kutoka katika eneo lake.