LDP kuanza tena majadiliano juu ya matumizi ya majina tofauti ya ukoo kwa wanandoa

Chama kikuu tawala nchini Japani cha Liberal Democratic, LDP kimeamua kuanzisha tena majadiliano ya ndani iwapo wanandoa waruhusiwe kutumia majina tofauti ya ukoo.

Kikosi kazi cha LDP kitaanza upya mjadala kuhusu suala hilo.

Uongozi wa chama hicho unaratibu kumteua Aisawa Ichiro aliyekuwa mkuu wa masuala ya Bunge kutoka LDP kuwa mwenyekiti wa timu hiyo. Nafasi hiyo ya uenyekiti imekuwa wazi.

Shirikisho la Biashara la Japani, au Keidanren, liliandaa pendekezo mapema mwezi huu ambalo linaitaka serikali kufanya mara moja marekebisho yanayohitajika kisheria ili kuruhusu chaguo la kutumia majina tofauti ya ukoo kwa wanandoa.

Wabunge wa LDP ambao wanaunga mkono mabadiliko hayo na wale walio na maoni ya tahadhari walifanya mikutano tofauti tangu Keidanren ilipoandaa pendekezo lake.

Uongozi wa LDP unapanga kutathmini kwa umakini suala hilo.