Mfalme wa Japani na Mkewe wawasili nchini Uingereza

Mfalme wa Japani Naruhito na Mkewe Masako wamewasili nchini Uingereza. Hii ni mara yao ya pili kufanya ziara ya ukarimu nje ya nchi tangu Mfalme Naruhito atawazwe mwaka 2019.

Ndege ya serikali iliyowabeba Mfalme na Mkewe ilitua katika uwanja wa ndege karibu na London muda mfupi baada ya saa 11:30 jioni jana Jumamosi.

Mfalme na Mkewe mara ya mwisho kuitembelea Uingereza ilikuwa wakati wa mazishi ya kitaifa ya Malkia Elizabeth II.

Kipindi hiki, walialikwa rasmi na Mfalme Charles. Leo Jumapili Mfalme anapanga kutembelea eneo la kuhamasisha utamaduni wa Japani jijini London.

Kesho kutwa Jumanne, Mfalme na Mkewe watahudhuria hafla ya kuwakaribisha pamoja na karamu katika Kasri la Buckingham.

Mfalme Naruhito anapanga kutembelea kaburi la familia ya kifalme ya Uingereza katika Kasri la Windsor Alhamisi wiki hii ili kuweka mashada ya maua katika kaburi la Malkia Elizabeth II na mumewe Mfalme Philip.

Siku inayofuata Mfalme Naruhito na Mkewe wamepangiwa kutembelea Chuo Kikuu cha Oxford mahali ambapo wote walisoma.