Japani yaadhimisha miaka 79 ya Mapigano ya Okinawa

Maadhimisho ya miaka 79 ya moja ya mapigano makali zaidi ya ardhini katika siku za mwisho za Vita Vikuu vya Pili vya Dunia yaliadhimishwa leo Jumapili katika mkoa wa Okinawa uliopo kusini magharibi mwa Japani.

Zaidi ya watu 200,000 walikufa, ikiwa ni pamoja na takribani moja ya nne ya raia wa Okinawa.

Okinawa inaitambua Juni 23, 1945 kama siku ya mwisho ya mapambano yaliyopangwa kati ya lililokuwa jeshi la Mfalme la Japani na vikosi vilivyoongozwa na Marekani.

Ibada ya kuwakumbuka waliokufa ilifanyika katika Bustani ya Kumbukumbu ya Amani katika mji wa Itoman, ambapo mapigano ya mwisho yalifanyika.

Jopo la wataalam wa Okinawa linasema idadi ya wakazi wa Okinawa ambao walipata tajiriba ya vita hivi sasa ni pungufu ya asilimia 10 ya idadi ya watu wa Okinawa.

Mwezi uliopita, picha mpya za video zilitolewa za makao makuu ya chini ya ardhi yaliyojengwa na Jeshi la Mfalme chini ya Kasri ya Shuri. Hapo ndipo inaaminika uamuzi mgumu ulitolewa ambao ulipelekea mauaji makubwa ya raia katika mkoa huo.

Wataalam wanasema kwamba njia za kuwasilisha uhalisia wa mapambano hayo kwa vijana zinafikia kipindi cha mageuzi kwa kuwa idadi ya manusura ambao wanaweza kuelezea tajiriba yao inapungua.

Wakazi wa Okinawa walikuwa na matumaini kuwa mkoa huo ungekuwa wa amani. Lakini takribani asilimia 70 ya kambi za Marekani nchini Japani bado zipo katika mkoa huo wa kusini magharibi.

Jukumu la Okinawa katika usalama wa Japani na mzigo uliopo kwa wakazi vyote vinaongezeka.

Serikali kuu inaendelea na mipango ya kuimarisha uwezo wa kujilinda wa taifa hilo katika visiwa vyake vya kusini magharibi, ikiwa ni pamoja na Okinawa.

Kuna mipango ya kuongeza vikosi vya Kikosi cha Kujilinda katika eneo hilo.