Wanandoa wa Kifalme wa Japani kuzuru Uingereza

Mfalme wa Japani Naruhito na Mkewe Masako wanaanza ziara ya siku nane nchini Uingereza kuanzia leo Jumamosi kama wageni wa kitaifa. Walialikwa rasmi na Mfalme Charles wa Uingereza.

Itakuwa ni ziara ya tatu ya kitaifa nchini Uingereza inayofanywa na Mfalme wa Japan na Mkewe. Ziara ya kwanza ilikuwa mwaka 1971, na ya pili mwaka 1998.

Ziara ya hivi karibuni ilipangwa mwaka 2020 kwa mwaliko wa hayati Malkia Elizabeth II wa Uingereza, lakini iliahirishwa kwa sababu ya janga la virusi vya korona.

Wanandoa hao wa Kifalme watahudhuria sherehe ya ukaribisho Jumanne wiki ijayo pamoja na karamu katika kasri la kifalme la Buckingham.

Mfalme Naruhito anapanga kuzuru kaburi la familia ya kifalme ya Uingereza katika kasri la Windsor Alhamisi ijayo kuweka shada la maua kwenye kaburi la Malkia Elizabeth II na mumewe Philip.

Siku itakayofuata, Mfalme na Mkewe wanatarajia kuzuru Chuo Kikuu cha Oxford, ambapo wote wawili walisoma hapo.