Watafiti wa Kijapani wamegundua rasilimali kubwa ya madini katika Bahari ya Pasifiki

Watafiti wa Kijapani wanasema wamegundua eneo lenye viwango vikubwa vya madini linaloitwa "manganese nodules” yaani “vinundu vya manganizi” kwenye Bahari nje ya kisiwa cha mashariki zaidi cha Japani katika Bahari ya Pasifiki.

Chuo Kikuu cha Tokyo na Taasisi ya Nippon Foundation zilitoa tangazo hilo katika mkutano na wanahabari jana Ijumaa jijini Tokyo.

Walisema timu ya utafiti ilichunguza zaidi ya maeneo 100 katika kina cha mita 5,500 kwenye bahari katika ukanda maalum wa kiuchumi wa Japani karibu na Kisiwa cha Minamitorishima kuanzia Aprili hadi Juni mwaka huu.

Timu hiyo ya utafiti iligundua eneo lenye vinundu vya manganizi vinavyofunika sakafu ya bahari. Inakadiria takriban tani milioni 230 za vinundu vya manganizi zipo katika hali rahisi kuchimba kama rasilimali.

Uchambuzi wa vinundu hivyo ulionyesha kuwa vinajumuisha madini ya chuma na manganizi, na pia vina kobalti na nikeli, ambazo hutumiwa katika kutengeneza betri za magari ya umeme.

Timu hiyo inakadiria kiasi cha kobalti kuwa takriban tani 610,000, sawa na miaka 75 ya matumizi ya kila mwaka ya Japani, na nikeli takriban tani 740,000, yenye thamani ya takriban miaka 11.

Chuo kikuu na taasisi hiyo zilitangaza mpango wa kuzindua mradi mkubwa wa majaribio ya kuvuna vinundu kwa ushirikiano na kampuni ya kigeni yenye rekodi ya maendeleo ya rasilimali za chini ya bahari.

Profesa wa Chuo Kikuu cha Tokyo na Mkurugenzi wa Taasisi ya Chiba ya Kituo cha Utafiti wa Rasilimali za Bahari kwa Kizazi Kijacho, Kato Yasuhiro, alisema anataka kuhakikisha mradi huo hautakuwa na athari kwa mazingira ya bahari, huku akiwasilisha data ambayo itakuwa ya kushawishi.