Putin: Urusi haiondoi uwezekano wa kuisambazia Korea Kaskazini silaha

Rais wa Urusi Vladimir Putin na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un walitia saini mkataba juzi Jumatano jijini Pyongyang. Maandishi yake yaliyowekwa wazi na Korea Kaskazini yanasema nchi hizo mbili zitatoa msaada wa pande mbili wa kijeshi ikiwa moja kati ya nchi hizo itawekwa katika hali ya vita kutokana na uvamizi wa kutumia silaha.

Putin alizungumza wakati wa mkutano na wanahabari katika mji mkuu wa Vietnam, Hanoi alioutembelea kufuatia ziara yake nchini Korea Kaskazini.

Aliulizwa na mwanahabari ikiwa unaweza ukachukuliwa kuwa uvamizi wa kutumia silaha ikiwa Ukraine itabainika kuwa ilishambulia maeneo yaliyopo katika eneo la Urusi kwa kutumia silaha zilizotolewa na nchi za Magharibi.

Putin alisema hali kama hiyo inakaribia hilo na Urusi inafanya tathmini. Pia alisema Urusi ina haki ya kusambaza silaha kwa sehemu zingine za dunia ikiwa ni pamoja na Korea Kaskazini.

Hata hivyo, Putin alisisitiza kuwa mkataba huo siyo tofauti na ule uliofikiwa kati ya Umoja wa Sovieti na Korea Kaskazini.

Matamshi hayo yanakinzana na tathmini ya Kim kuwa uhusiano kati ya Korea Kaskazini na Urusi umefikia kiwango cha ushirikiano. Urusi haijatoa yaliyomo kwenye mkataba huo.