Korea Kusini yashutumu mkataba wa Korea Kaskazini na Urusi, huenda ikaipatia Ukraine silaha

Korea Kusini imezishutumu Urusi na Korea Kaskazini kwa kutiliana saini mkataba unaoahidi msaada wa pande mbili wa kijeshi iwapo nchi mojawapo itashambuliwa. Afisa mwandamizi wa Korea Kusini pia ameashiria uwezekano wa Korea Kusini kubadili msimamo wake kuhusu kuipatia silaha Ukraine.

Ofisi ya Rais wa Korea Kusini iliitisha mkutano wa Baraza la Usalama la Taifa jana Alhamisi kuujadili mkataba huo na kutoa tamko.

Tamko hilo linaelezea wasiwasi mkubwa juu ya mkataba huo, unaolenga kuimarisha ushirikiano wa kijeshi na kiuchumi kati ya Urusi na Korea Kaskazini.

Tamko hilo linasema kuwa ushirikiano wowote unaosaidia moja kwa moja au kwa namna isiyo ya moja kwa moja uimarishaji wa kijeshi wa Korea Kaskazini ni ukiukaji wa maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Afisa mwandamizi wa ofisi ya Rais ya Korea Kusini amewaambia wanahabari jana Alhamisi kuwa serikali inapanga kuangalia upya suala la kuipatia Ukraine msaada wa kijeshi. Maoni hayo yanaashiria uwezekano wa Korea Kusini kubadili sera yake ya kutoipatia Ukraine silaha za maangamizi.