Putin atafuta kuimarisha uhusiano na Vietnam

Rais wa Urusi Vladimir Putin amezuru Vietnam na kufanya mazungumzo na Rais wa nchi hiyo To Lam jana Alhamisi. Viongozi hao walikubaliana kuimarisha ushirikiano wa pande mbili kwenye nyanja kama vile biashara na nishati.

Putin alisema kuwa anataka nchi hizo mbili ziwe na ushirikiano thabiti wa kimkakati.

Akizungumza katika mkutano wa pamoja na wanahabari, alisema kuwa biashara baina ya nchi hizo mbili tayari imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 30 mwaka huu. Pia alisema kampuni za Urusi zipo tayari kushiriki katika miradi mikubwa ya gesi asilia ya kimiminika nchini Vietnam.

Pande hizo mbili zimekuwa na uhusiano wa karibu tangu enzi za Umoja wa Kisovieti. Hata hivyo, uhusiano huo haujaizuia Vietnam dhidi ya kuimarisha pia uhusiano na Marekani na Japani hasa katika nyanja za uwekezaji na biashara.

Putin baadaye alikutana na kiongozi wa ngazi ya juu wa Vietnam ambaye ni Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomunisti Nguyen Phu Trong.