Vyombo vya habari vya Israel vyaripoti ‘mivutano’ kati ya serikali ya Netanyahu na maafisa wa ulinzi

Msemaji wa Vikosi vya Ulinzi vya Israel, IDF Daniel Hagari juzi Jumatano alizungumza katika mahojiano na runinga moja nchini humo.

Hagari alisema “kazi hii ya kuangamiza Hamas” ni “kurusha mchanga katika macho ya umma.” Alisema Hamas ni wazo ambalo limejikita katika mioyo ya watu, na kwamba “yeyote anayefikiria tunaweza kuangamiza Hamas amekosea.”

Hagari pia aliripotiwa kusema operesheni ya kijeshi peke yake haitawarejesha mateka wote, kwa hivyo njia mbadala lazima ipatikane ili kuhakikisha kurejea kwao.

Ofisi ya Waziri Mkuu ilitoa taarifa iliyoashiria kutoridhika kabisa na maoni ya Hagari. Ilisema Baraza la Mawaziri limeweka uangamizaji wa uwezo wa kijeshi na kiutawala wa Hamas kuwa moja ya malengo ya vita.

Ripoti za vyombo vya habari vya Israel kuhusu kuongezeka kwa mivutano kati ya utawala wa nchi hiyo na viongozi wa IDF zimekuja baada ya Waziri wa zamani wa Ulinzi Benny Gantz kujiuzulu kutoka kwenye Baraza la Mawaziri la Vita mapema mwezi huu. Kuondoka kwake kulisababisha kuvunjwa kwa baraza hilo. Hii ilichukuliwa kuwa ishara nyingine ya kuongezeka kwa mivutano ndani ya Israel.