Putin na Kim waahidi kusaidiana kijeshi katika mkataba mpya

Viongozi wa Urusi na Korea Kaskazini wamefanya mkutano wa pamoja na wanahabari baada ya kutia saini mkataba mpya unaojumuisha ahadi ya pande mbili ya kusaidiana kijeshi.

Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema, “Mkataba uliosainiwa unasema kwamba nchi zetu zitasaidiana ikiwa moja wapo itashambuliwa.”

Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un amesema, “Najivunia kuwa tumekuja na mkataba wa kimkakati unaoendana na zama mpya.”

Wawili hao walifanya mkutano jana Jumatano jijini Pyongyang.

Katika maoni yake ya ufunguzi, Kim alisisitiza kwamba anaunga mkono uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

Putin alisema mkataba huo mpya uliosainiwa unaweza kupanua mabadilishano ya teknolojia ya kijeshi kati ya Urusi na Korea Kaskazini. Kadhalika ameahidi kuwa nchi hizo mbili zitaungana kukabiliana na vikwazo vya muda mrefu vya nchi za magharibi.

Chombo cha habari cha serikali ya Urusi kimeripoti kwamba Putin amewasili nchini Vietnam baada ya kumaliza ziara yake nchini Korea Kaskazini.