Japani kuruhusu wakurufunzi wa kigeni kutoa huduma ya uuguzi ya kutembelea majumbani

Wizara ya Afya, Kazi na Ustawi wa Jamii ya Japani imeamua kuwaruhusu raia wa kigeni katika programu za mafunzo ya kiufundi na wafanyakazi maalum wenye ujuzi kutoa huduma ya uuguzi ya kutembelea majumbani, kutatua uhaba mkubwa wa watoa huduma nchini humo.

Kwa sasa, idadi ndogo ya raia wa kigeni walioidhinishwa kama wafanyakazi wa huduma wanaruhusiwa kutoa huduma ya uuguzi ya kutembelea majumbani, inayofanywa na mfanyakazi mmoja.

Wakurufunzi wa kigeni na wafanyakazi maalum wenye ujuzi walio na hadhi za ukaazi hawaruhusiwi kujihusisha kwenye sekta hiyo.

Jopo la wizara hiyo jana Jumatano liliidhinisha mpango wa kuwaruhusu kuwa wahudumu wa kutembelea majumbani iwapo watakidhi masharti fulani.

Hususan, waombaji nafasi hizo watalazimika kukamilisha kozi ya mafunzo kwa wanaoanza juu ya mbinu za kuhudumia.

Waajiri pia watahitajika kuwafunza kuhusu maisha ya Kijapani na njia za mawasiliano, na wafanyakazi wao waandamane nao kwa ajili ya mazoezi halisi kwa kipindi fulani.

Maafisa wa wizara watawatembelea waajiri kuchunguza iwapo watu wanafundishwa ipasavyo, na wataanza huduma ya ushauri kwa wahudumu raia wa kigeni ili kuzuia na kushughulikia unyanyasaji unaowezekana.

Wizara imepanga kuomba maoni ya umma juu ya mpango huo, na kuanza utekelezaji katika mwaka wa fedha wa 2025 ikiwa ni mapema zaidi, utakaoanza mwezi Aprili mwakani.