Kim na Putin watarajiwa kutia saini mkataba wa ushirikiano wa kimkakati

Televisheni inayoendeshwa na serikali ya Korea Kaskazini imerusha picha za video za kiongozi mkuu wa nchi hiyo Kim Jong Un akimpokea Rais wa Urusi Vladimir Putin wakishikana mikono na kukumbatiana katika uwanja wa ndege jijini Pyongyang mapema leo Jumatano.

Picha hizo pia zilionyesha Kim na Putin wakiwa pamoja wamepanda katika gari ya rais wa Urusi. Msafara wao ulipita kwenye mitaa iliyokuwa imepambwa kwa bendera ya Urusi na picha ya Putin na kuelekea Nyumba ya Wageni wa Kitaifa ya Kumsusan.

Ziara ya Putin nchini Korea Kaskazini ni ya kwanza katika kipindi cha miaka 24. Kim na Putin mara ya mwisho walikutana Mashariki ya Mbali ya Urusi mwezi Septemba mwaka 2023.

Mkutano huu wa sasa wa viongozi hao unakuja wakati Urusi ikishutumiwa kupata makombora ya balistiki ya masafa mafupi na risasi za mizinga kutoka Korea Kaskazini ili kuzitumia nchini Ukraine. Yenyewe Korea Kaskazini inasemekana kupokea chakula, nishati na msaada mwingine kutoka Urusi.

Kim na Putin wanatarajiwa kutia saini mkataba wa ushirikiano wa kimkakati, ili kuainisha mahusiano imara ya pande mbili ili kukabiliana na Marekani na maadui wengine.