Mahojiano ya NHK: Mtoto wa Aung San Suu Kyi aomba nchi zingine kumsaidia mama yake

Kiongozi wa kidemokrasia wa Myanmar Aung San Suu Kyi ametimiza miaka 79 jana Jumatano. Mshindi huyo wa Tuzo ya Amani ya Nobel amekuwa akizuiliwa na jeshi la Myanmar tangu wanajeshi walipochukua mamlaka katika mapinduzi ya mwaka 2021.

Mwanawe, Kim Aris kwa sasa anaishi Uingereza. Katika mahojiano na NHK alisema hana uhakika ni wapi mama yake alipo.

Alisema yeye na wafuasi wa mama yake wanasikia mara kwa mara kwamba amehamishwa kutoka gerezani hadi katika aina fulani ya kifungo cha nyumbani, lakini wanasikia kwamba habari hiyo sio sahihi. Hivyo, kwa sasa, wanaamini kuwa bado yuko gerezani huko Naypyidaw.

Alisema baadaye alipokea "barua yenye mwandiko wake" mnamo Januari. Alisema barua hiyo ni ya kwanza kuona au kusikia kutoka kwa mamake katika kipindi cha miaka mitatu na nusu iliyopita

Kuhusiana na hali ambapo vikundi vinavyounga mkono demokrasia vinatumia nguvu kupigana na jeshi, alisema, "iwe ni njia sahihi au la, inaweza kuwa njia pekee kwa sasa."

Aris alisema mama yake amekuwa akisimamia maridhiano ya amani na kujaribu kufanya mambo kwa umwagaji wa damu mdogo iwezekanavyo. Alisema “atakuwa anahuzunika sana" kujua kinachotokea sasa.

Aris alisema mama yake “pamoja na watu wengi wamefungwa bila sababu yoyote isipokuwa kuamini katika haki za binadamu. "Alizitaka nchi zingine zisikae kimya.

Alisema anadhani jumuiya ya kimataifa inaweza kufanya mengi zaidi kuzuia upatikanaji wa vifaa kama vile usafiri wa anga na mafuta kwa jeshi la Myanmar.

Alisema watu wa nchi zingine, ikiwemo Japani, wanapaswa kuweka shinikizo kwa serikali zao kuchukua hatua za maana na kuendelea kuunga mkono demokrasia nchini Myanmar.