Mkuu wa UN wa Upunguzaji Hatari za Majanga atoa wito wa kuwepo kwa mfumo wa tahadhari wa usawa wa kijinsia

Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa, UN ya Kupunguza Hatari za Majanga amesisitiza umuhimu wa kuweka mfumo wa tahadhari ambao unampa kila mtu fursa ya kupata taarifa. Alisema wanawake wengi hupata athari kuliko wanaume katika majanga ya asili kwa sababu wanashindwa kupata taarifa za tahadhari mapema.

Mwakilishi Maalum wa Kupunguza Hatari za Majanga Kamal Kishore alizungumza na NHK katika mahojiano jijini Tokyo nchini Japani juzi Jumanne.

Kishore alisema “Mabadiliko ya tabia nchi yanaongeza majanga," yanaathiri sio tu maisha ya watu na riziki, lakini pia tamaduni nzima kwani jamii zinalazimika kuhama.

Kishore alibainisha kuwa wanawake wanateseka zaidi kuliko wanaume katika nchi ambazo ushiriki wa wanawake katika jamii uko nyuma. Alisema, kwa mfano, ikiwa wanawake wanatunza kaya wakati wanaume wanafanya kazi, wanaweza kuwa wa mwisho kusikia kimbunga kinapokaribia.

Alisema ni muhimu wanawake na wazee kuchangia mawazo yao wakati wa kuweka mfumo wa kuzuia majanga.

Kishore alisema, "kuna mengi ya kujifunza kutoka Japani." Alisema nchi hiyo imekuwa kiongozi, ikishirikisha uzoefu wake "kwa dunia kwa ukarimu sana na kwa uwazi sana. Na hiyo inaleta mabadiliko makubwa duniani.”