Biden kuwapa wenza wasio na hati za uraia wa Merekani njia rahisi ya ukazi

Rais wa Marekani Joe Biden ametangaza kuwa atawarahisishia wakazi wa muda mrefu wasio na hati za uraia waliooana na raia wa Marekani kuomba ukazi wa kudumu.

Mchakato huo mpya utatumika kwa watu walioingia Marekani kinyume cha sheria, waliooana na raia wa Marekani, na wameishi nchini humo kwa muda usiopungua miaka 10.

Wataruhusiwa kuomba ukazi halali wa kudumu bila kulazimika kuondoka nchini humo.

Sheria za sasa zinawataka waombaji kuondoka Marekani wakati kesi zao zikishughulikiwa. Hii imezilazimu familia zilizoathiriwa kuishi mbalimbali kwa miaka mingi.

Sera ya uhamiaji imekuwa moja ya masuala muhimu katika uchaguzi wa rais wa mwezi Novemba, huku kukiwa na wimbi kubwa la wahamiaji wanaojaribu kuvuka mpaka wa kusini wa Marekani.

Biden hivi karibuni alikabiliwa na msukosuko kutoka kwa wafuasi wa chama cha Democrat alipoamuru kusitisha kushughulikia madai ya ukazi wakati uvukaji haramu wa mpaka kutoka Mexico ukifikia viwango fulani vya juu.

Hatua nafuu ya hivi karibuni ya rais inaonekana inalenga kuwaweka upande wake wapiga kura wenye mawazo huru.