Marekani, Ufilipino zalaani kitendo cha China katika Bahari ya China Kusini

Marekani na Ufilipino zimeishutumu China kwa “kitendo hatari” katika Bahari ya China Kusini ambacho kinatishia amani na uthabiti katika eneo la Indo-Pasifiki.

Kujihusisha kwa Marekani kunakuja baada ya Ufilipino kudai jukumu la kusambaza bidhaa la moja ya meli zake kutatizwa na meli za China katika eneo la bahari linalozozaniwa.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Kurt Campbell alizungumza kwa njia ya simu na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufilipino Maria Theresa Lazaro juzi Jumatatu.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Marekani alisema mataifa hayo mawili yana wasiwasi wa pamoja juu ya “vitendo vinavyoongezeka na visivyo vya uwajibikaji” vya China.

Serikali ya Ufilipino inasema meli ya China, walinzi wa pwani na vyombo vya usafiri baharini vya jeshi vilizuia jukumu lake la kusambaza tena bidhaa kwenye kambi ya jeshi katika sehemu ya kina kifupi cha bahari ya Second Thomas juzi Jumatatu.

Jeshi la majini la Ufilipino pia lilisema afisa mmoja alijeruhiwa vibaya kutokana na kugongwa kwa kasi na kwa makusudi na meli ya China.

Eneo la bahari karibu na kina kifupi linadhibitiwa na Ufilipino, lakini China inadai umiliki wake.
Walinzi wa pwani wa China walisema meli ya kusambaza bidhaa ya Ufilipino iliingia kinyume cha sheria katika eneo la maji karibu na kina hicho. Iliishutumu meli hiyo kwa makusudi kukaribia meli yake, na kupelekea kugongana kidogo.

Mwezi Machi, walinzi wa pwani wa China walifyatua mizinga ya maji dhidi ya meli za Ufilipino katika Bahari ya China Kusini, na kusababisha majeruhi.