Japani, Marekani, Ufilipino na Canada zafanya mazoezi ya pamoja katika Bahari ya China Kusini

Kikosi cha Kujihami cha Majini cha Japani, MSDF kinasema kimefanya mazoezi ya pamoja na Marekani, Ufilipino na Canada katika Bahari ya China Kusini.

Mazoezi hayo yaliyofanyika juzi Jumapili yalihusisha manowari ya MSDF, manowari ya jeshi la majini la Marekani, meli ya doria kutoka jeshi la majini la Ufilipino na manowari ya Jeshi la Kifalme la Majini la Canada.

Maafisa wanasema hii ni mara ya kwanza kwa nchi hizo nne kufanya kile wanachokiita “Shughuli ya Ushirikiano wa Baharini” pamoja. Vyombo vilivyoshiriki vilifanya shughuli mbalimbali kupima uratibu wao, ikiwa ni pamoja na mawasiliano na mafunzo ya kuongoza vyombo baharini.

Hii inakuja wakati ambapo China imeongeza shughuli zake baharini, ambapo meli za Ufilipino zimesumbuliwa mara nyingi na meli za doria za China.