Israel yaendeleza mashambulizi Gaza, yatangaza kusitisha kwa ajili ya misaada

Israel imeendelea na mashambulizi katika Ukanda wa Gaza huku ikitangaza kusitisha kwa muda shughuli yake ya kijeshi kwenye eneo la kusini ili kuruhusu misaada zaidi ya kibinadamu kuingia ukanda huo.

Jana Jumapili jeshi la Israel lilisema kuwa usitishaji huo utajumuisha njia ya kutoka Kerem Shalom mpaka kwenye barabara muhimu na kaskazini zaidi. Njia hiyo inaweza kutumiwa kupitisha misaada ya kibinadamu hadi mji wa Khan Younis kusini mwa Gaza.

Jeshi hilo limesema usitishaji huo wa vita utaanza saa mbili asubuhi hadi saa moja jioni kila siku mpaka watakapotoa tena taarifa zaidi.

Lakini jeshi hilo limeandika katika mtandao wa kijamii kwamba litaendelea na operesheni kusini mwa Gaza, ikiwa ni pamoja na Rafah. Ujumbe huo ulioandikwa kwa Kiebrania ni wazi unataka kuwaonyesha Waisrael kuwa jeshi hilo litadumisha msimamo wake mkali.

Jeshi la Israel limeendelea na mashambulizi kote eneo la Gaza jana Jumapili. Chombo kimoja cha habari kwenye eneo hilo kimesema bomu lililolenga makazi mawili katika kambi ya wakimbizi katikati mwa Gaza limeua watu sita, akiwemo mtoto mdogo na kujeruhi makumi kadhaa.

Maafisa wa afya wa Gaza wamesema idadi ya vifo kwenye eneo hilo imeongezeka hadi 37,337 tangu kuanza kwa mapigano Oktoba mwaka jana.