Lai: Kazi ya jeshi la Taiwan ni kulinda amani kwenye mlango bahari wa Taiwan

Rais wa Taiwan Lai Ching-te anasema kazi kubwa zaidi ya jeshi la Taiwan ni kuchukua jukumu kubwa la kudumisha amani na uthabiti kwenye Mlango Bahari wa Taiwan.

Lai alizungumza hayo katika hafla ya miaka 100 ya chuo cha jeshi mjini Kaohsiung kusini mwa Taiwan.

Chuo hicho kilianzishwa nchini China mwaka 1924 na chama cha Kuomintang. Kilihamishiwa Kaohsiung baada ya chama hicho kushindwa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe dhidi ya Chama cha Kikomunisti cha China.

Katika hotuba yake kwa maafisa wanafunzi, Lai alisema jeshi la sasa si la mtu binafsi wala chama chochote, bali ni tiifu kwa Taiwan, watu na demokrasia.

Maoni yake yalijikita katika wazo kuwa Taiwan ni tofauti na China. Alizungumzia hilo pia katika hotuba yake ya kula kiapo Mwezi Mei.

Katika kujibu hilo, China imefanya mazoezi makubwa ya kijeshi jirani na Mlango Bahari wa Taiwan kuonyesha kuwa inapinga.