Filamu ya Kijapani yashinda tuzo katika tamasha la kimataifa la filamu za anime nchini Ufaransa

Filamu ya Kijapani ya “Totto-chan: The Little Girl at the Window” imeshinda moja ya tuzo za juu kwenye Tamasha la Filamu za Anime la Kimataifa la Annecy nchini Ufaransa.

Tamasha hilo lilivutia washiriki wengi waliowakilisha kazi zikiwemo filamu ndefu na fupi za anime kushindana kuwania tuzo ya juu, Crystal Award.

Filamu ya Kijapani ilishinda Tuzo ya Paul Grimault katika kipengele cha filamu ndefu jana Jumamosi. Iliandikwa na kuongozwa na Yakuwa Shinnosuke.

Imejikita kwenye riwaya ya wasifu wa muigizaji maarufu wa Kijapani na mtangazaji wa televisheni Kuroyanagi Tetsuko.

Riwaya hiyo iliyochapishwa mwaka 1981, ilipata mauzo makubwa na imetafsiriwa katika lugha nyingi.

Filamu hiyo inaelezea maisha ya utotoni ya msichana mdogo aitwaye Totto-chan wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia jijini Tokyo. Inaonyesha namna msichana mwenye furaha alivyoathiriwa na vita.

Filamu hiyo inaangazia kipindi ambapo msichana ameondolewa shule ya msingi kwa sababu alishindwa kukaa darasani na alipelekwa shule nyingine iitwayo Tomoe, alipopata marafiki.

Shule ya Tomoe ni ya kipekee, ambapo behewa la treni linatumika kama darasa.

Mkuu wa shule anawafuatilia wanafunzi wake kwa bashasha na mapenzi.

Mwigizaji Yakusho Koji, aliyeshinda Tuzo ya Mwigizaji Bora katika Tamasha la Kimataifa la Filamu la Cannes mwaka 2023 kwa kazi yake kwenye filamu ya “Perfect Days”, aliigiza sauti ya mkuu wa shule kwenye filamu hiyo.

Mwaka jana, filamu nyingine ndefu ya anime ya Kijapani “The Tunnel to Summer, the Exit of Goodbyes” iliyoongozwa na Taguchi Tomohisa, ilishinda Tuzo ya Paul Grimault kwenye tamasha hilo.