Zelenskyy asisitiza umuhimu wa washiriki katika mkutano wa amani

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenksyy amesisitizia umuhimu wa idadi ya mataifa ambayo yamekusanyika katika mkutano wa kimataifa ili kujadili kuleta amani katika nchi yake.

Mkutano huo wa kujadili mpango wa amani uliopendekezwa na Ukraine ulianza jana Jumamosi katika eneo la kitalii la Burgenstock lililopo nchini Uswisi. Wajumbe kutoka takribani mataifa na taasisi za kimataifa 100 wanashiriki mkutano huo.

Viongozi wa mataifa wanaoshiriki mkutano huo ni pamoja na Waziri Mkuu wa Japani Kishida Fumio, Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron.

Zelenskyy alisema, “Tumefanikiwa kuepuka moja ya vitu vibaya zaidi, ambacho ni kuigawa dunia katika makundi yanayopingana.”

Washiriki wa mkutano huo ni pamoja na mataifa kutoka kile kinachofahamika kuwa ni Global South na yana uhusiano na Urusi, lakini Urusi haishiriki mkutano huo.

Rais Zelenskyy alisema Ukraine itashirikiana na mataifa yanayoshiriki mkutano huo kuandaa mpango kazi ambayo utawasilishwa kwa wawakilishi wa Urusi.

Alielezea matumaini yake ya “kumaliza kabisa vita” katika mkutano wa viongozi wa pili wa amani.

Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris alilitaja pendekezo lililotolewa juzi Ijumaa na Rais Vladimir Putin wa Urusi, ikiwa ni pamoja na masharti yake ya kuanza mazungumzo ya amani.

Harris alisema, “Hataki kufanya majadiliano, anataka kujisalimisha.”

Katika hatua nyingine, Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia Mwanamfalme Faisal bin Farhan Al Saud alisema majadiliano ya kina yatahitaji “maelewano magumu" na kwamba ushiriki wa Urusi katika mchakato mzuri ni muhimu ili kufikia amani.