Maafisa wa hali ya hewa wa Japani waonya juu ya joto kali na unyevunyevu leo Jumapili

Maafisa wa hali ya hewa leo Jumapili wanaonya kuwepo kwa hali ya joto kali na unyevunyevu kote nchini Japani, kufuatia hali ya joto iliyorekodiwa katika maeneo mengi ya nchi hiyo jana Jumamosi.

Mamlaka ya Hali ya Hewa imesema hali ya jua iliyoongeza halijoto jana Jumamosi hadi katika viwango vya katikati ya msimu wa joto kali, hasa katika maeneo kando ya Bahari ya Japani.

Mji wa Nagaoka uliopo katika Mkoa wa Niigata uliandikisha halijoto kubwa ya nyuzijoto 35.4 za selsiyasi.

Halijoto kubwa ya kawaida ambayo hutokea katika nusu ya kwanza ya mwezi Julai ilionekana pia katika baadhi ya majiji makubwa. Osaka ilikuwa na nyuzijoto 30.6, Fukuoka ilirekodi nyuzijoto 30.2, Nagoya ilishuhudia nyuzijoto 30 na katikati mwa Tokyo kulikuwa na nyuzijoto 29.9

Idara ya Zimamoto ya Tokyo imesema kwamba hadi kufikia saa tatu usiku jana Jumamosi, watu 18 katika jiji hilo walipelekwa hospitali kutokana na ugonjwa wa joto kali.

Maafisa wa hali ya hewa wanatabiri halijoto ya takribani nyuzijoto 30 kote nchini humo kutokea tena leo Jumapili, na wanaonya kwamba viwango vya unyevunyevu pia vitaongezeka.

Wanatoa wito kwa watu kuchukua hatua za kuzuia ugonjwa wa joto kali kwa kutumia viyoyozi pale inapohitajika, kunywa maji, kuepuka kufanya kazi kwa muda mrefu ama kufanya mazoezi magumu nje na kupumzika pale inapohitajika.

Maafisa hao wanasema leo Jumapili hali ya angahewa inayobadilika badilika huenda ikatokea katika maeneo mengi kuanzia magharibi hadi kaskazini mwa Japani. Wanawashauri watu kuchukua tahadhari ya radi, upepo mkali ikiwa ni pamoja na vimbunga pamoja na mvua kubwa ya mawe.