Toyota kuongeza muda wa kusitisha uzalishaji wa aina za magari zilizokumbwa na kashfa hadi angalau Julai 31

Kampuni ya Toyota Motor imeamua kuendelea kusimamisha uzalishaji wa aina tatu zilizoathiriwa na upotoshaji wa data za majaribio hadi Julai au baadaye, zaidi ya muda uliowekwa wa awali wa Juni 28.

Toyota inasema haijaamua ni lini itarejelea uzalishaji huo lakini kusimamishwa kutasalia angalau hadi Julai 31.

Mapema mwezi huu Toyota ilibainika kuwa na majaribio ya uwongo ya utendakazi ili kupata uthibitisho wa serikali kwa magari yake.

Wizara ya usafirishaji iliamuru Toyota kusimamisha kupelekea shehena kwa magari yaliyoathiriwa.

Toyota iliacha kuzalisha Yaris Cross na miundo mingine miwili kwenye viwanda vyake vilivyopo mikoa ya Miyagi na Iwate kuanzia Juni 6.

Kampuni hiyo ilisema pia imesitisha upimaji na taratibu zingine ambazo ni muhimu ili kupata uthibitisho wa serikali kwa aina mpya inazopanga kuuza.

Toyota inasema hii ilisababisha kuahirisha mauzo yaliyokusudiwa katikati ya mwaka 2024 ya gari mpya la kifahari la Crown.

Maafisa wa wizara ya usafirishaji walifanya ukaguzi kwenye viwanda vya Toyota, Mazda, Yamaha, Honda na Suzuki juu ya mfululizo wa upotoshaji wa data za majaribio.

Mazda pia imesitisha kutengeneza Mazda2 na aina nyingine ya gari kwenye kiwanda kilichopo mikoa ya Hiroshima na Yamaguchi tangu Juni 6.

Wasiwasi unaongezeka kuhusu athari ya kusimamishwa kwa uzalishaji kwenye uchumi wa ndani na washirika wa biashara.