Benki Kuu ya Marekani haijabadilisha viwango vya riba

Watunga sera katika Benki Kuu ya Marekani wanasema mfumuko wa bei umeshuka kufikia kiwango chao wanacholenga lakini waliamua kutobadilisha viwango vya riba. Wameashiria kuwa watapunguza kiwango hicho mara moja tu mwaka huu.

Benki kuu hiyo imetoa tangazo hilo baada ya kufunga mkutano wake wa sera wa siku mbili jana Jumatano.

Wakuu wa benki hiyo walipandisha viwango vya riba ili kuwakatisha tamaa watumiaji na wafanyabiashara ya kukopa baada ya mfumuko wa bei kufikia viwango vya juu ambavyo havijawahi kutokea katika miongo kadhaa.

Tangu Julai mwaka jana, kiwango cha riba kimekuwa katika asilimia 5.25-5.50.

Ingawa mfumuko wa bei umeshuka hadi chini ya nusu ya kiwango cha kilele chake, maafisa wanasema uendelezaji zaidi unahitajika.

Mwenyekiti wa Benki Kuu Jerome Powell alisema, “Hatudhani kama itakuwa vizuri kupunguza viwango na kuanza kulegeza sera hadi tuwe na imani zaidi kwamba mfumuko wa bei unarudi chini hadi asilimia 2 kwa msingi endelevu."

Makadirio yao mapya yanaonyesha kiwango cha riba cha benki hiyo kitakuwa asilimia 5.1 mwishoni mwa mwaka. Hiyo inaashiria punguzo la robo moja ya asilimia ya alama kwa mwaka, ambayo ni chini ya mbili kutoka utabiri wa awali wa mwezi Machi.