Blinken ashinikiza Israel na Hamas kukubali kusitisha vita

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken amerejea Mashariki ya Kati kujaribu kuokoa mpango wa hivi karibuni wa kusitisha vita. Alikutana na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu mjini Jerusalem jana Jumatatu na kusisitiza umuhimu wa kufuata pendekezo hilo.

Mpango huo wenye awamu tatu unaanza na usitishaji vita utakaodumu wiki sita. Hamas itawaachilia mateka wote. Kisha, Israel itaviondoa vikosi vyake eneo la Gaza ili kuruhusu watu kufanya ujenzi mpya.

Netanyahu amesema vikosi vyake vimedhamiria kupata “ushindi kamili,” na amedhamiria “kuiangamiza Hamas.”

Blinken alimwambia Netanyahu kuwa pendekezo hilo “litafungua” uwezekano wa utulivu kwa raia wa Israel na “utangamano zaidi” katika eneo hilo.

Blinken amekuwa akitoa wito kwa watu katika eneo hilo lote kuwashinikiza viongozi wa Hamas. Alisema, “karibu dunia yote” inaunga mkono pendekezo hilo, lakini upande pekee ambao haujasema “ndio” ni Hamas.

Jumamosi wiki iliyopita, viongozi wa Hamas walitoa taarifa wakisema hawawezi wakakubali usitishaji wowote wa vita hadi vikosi hivyo vya Israel viondoke na kumaliza kuzingira kwao.