Baraza la Usalama la UN laidhinisha azimio la kusitisha vita Gaza

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeidhinisha azimio linalotoa wito kwa pande zote za Israel na Hamas kukubali mpango mpya wa kusitisha vita uliotangazwa na Rais wa Marekani Joe Biden.

Mei 31 mwaka huu, Biden alitangaza pendekezo la awamu tatu linalojumuisha usitishaji vita kwa wiki sita katika Ukanda wa Gaza na kuachiliwa kwa mateka.

Marekani iliwasilisha rasimu ya azimio kwa Baraza la Usalama linalotoa wito wa kuungwa mkono kwa pendekezo hilo.

Jana Jumatatu, nchi 14 kati ya 15 wanachama wa baraza hilo ikiwemo Japani na China zilipiga kura kuidhinisha azimio hilo. Urusi haikutumia kura yake ya turufu kulipinga na haikupiga kura.

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, UN Linda Thomas-Greenfield alisema “Baraza hili limetuma ujumbe bayana kwa Hamas: Kubali mpango wa kusitisha vita uliopendekezwa.”

Aliongeza kuwa kwa sababu Israel tayari imekubali mpango huo, mapigano yanaweza yakasitishwa leo ikiwa Hamas itaukubali pia.”

Balozi wa Urusi huko UN Vassily Nebenzia alikiri kuwa kuna haja ya vita kusitishwa, lakini alitilia shaka ikiwa Israel kwa kweli imekubali kusitisha vita kama Marekani inavyosisitiza.