Taarifa ya pamoja kwenye mkutano wa amani huenda isijumuishe kuondolewa kwa vikosi vya Urusi

NHK imebaini kwamba rasimu ya taarifa ya pamoja ambayo haijatoa wito wa kuondolewa kwa vikosi vya Urusi itawasilishwa kwenye mkutano ujao wa kimataifa wa amani ya Ukraine.

Mkutano huo wa viongozi wakuu kuhusu amani utafanyika nchini Uswizi Jumamosi na Jumapili wiki hii. Unalenga kufanikisha mpango wa amani wenye hoja 10 ambao umependekezwa na Ukraine.

Serikali ya Uswizi jana Jumatatu ilisema kwamba nchi na mashirika 90 yanatarajiwa kushiriki mkutano huo.

NHK imepata rasimu ya taarifa hiyo ya pamoja ambayo inataja hoja tatu pekee kati ya 10 zilizopendekezwa na kamati ya amani ya Ukraine.

Hoja hizo tatu ni usalama wa mitambo ya nyuklia, usalama wa chakula na kuachiliwa kwa wafungwa wote na kurejeshwa kwa watoto waliopelekwa Urusi.

Taarifa hiyo haijataja kuondolewa kwa vikosi vya Urusi nchini Ukraine na kurejeshwa kwa uadilifu wa maeneo ya Ukraine.

Vyanzo vya habari vya kidiplomasia vinasema kwamba kuondolewa kwa vikosi vya Urusi na vitu vingine ambavyo Ukraine imekuwa ikitoa wito vifanywe viliondolewa kwenye rasimu hiyo kwa sababu ilizingatia baadhi ya nchi zinazoibukia barani Asia na Mashariki ya Kati zinazodumisha uhusiano na Urusi.