Urusi yaishukuru China kwa kutohudhuria mkutano wa amani wa Ukraine

Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergey Lavrov ameelezea shukrani zake kwa China kwa kutohudhuria mkutano wa amani ya Ukraine nchini Uswizi. Aliyasema hayo alipokutana na mwenzake wa China Wang Yi.

Lavrov na Wang wamekutana pembezoni mwa mkutano wa siku mbili wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa BRICS ulioanza jana Jumatatu mjini Nizhny Novgorod nchini Urusi.

Urusi imeshutumu mkutano huo wa amani ya Ukraine, kwa kuwa unafanyika bila Urusi kushiriki. Mwezi uliopita, China ilitangaza nia yake ya kutoshiriki mkutano huo.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi ilimnukuu Lavrov akimwambia Wang kuwa Urusi inashukuru kutokana na msimamo wenye uwiano na usioyumba wa China kwenye mzozo nchini Ukraine.

Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Wang alisisitiza kwamba China inaunga mkono kikamilifu jukumu la Urusi kama mwenyekiti wa BRICS. Aidha Wang alisema China itafanya kazi na Urusi kukuza umoja na kujiboresha kwa nchi zinazoibukia na zinazoendelea ambazo kwa pamoja zinazojulikana kama Global South.

Wang alisisitiza msimamo wa China kuwa nchi hiyo itafanya kazi kuimarisha ushirikiano na nchi za Global South chini ya mpangokazi wa BRICS kwa lengo la kukabiliana na nchi za Magharibi.