Belarus yajiunga na mazoezi ya kimbinu ya nyuklia ya Urusi

Wizara ya Ulinzi ya Belarus ambayo ni mshirika wa Urusi inasema vikosi vyake vinashiriki mazoezi ya kijeshi ya Urusi ili kuigiza kuwekwa tayari kwa silaha za kimbinu za nyuklia.

Wizara hiyo jana Jumatatu ilisema vikosi kutoka jeshi la Belarus vinashiriki awamu ya pili ya mazoezi ya Urusi.

Wizara ya Ulinzi ya Urusi mwishoni mwa mwezi jana ilitangaza kuanza kwa awamu ya kwanza ya mazoezi hayo katika Eneo la Kijeshi la Kusini ambalo pia linatumika kama kambi ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine. Belarus ilitarajiwa kujiunga na awamu ya pili.

Ingawa silaha za kimbinu za nyuklia za Urusi zimepelekwa nchini Belarus, hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Belarus kushiriki mazoezi yanayohusisha silaha kama hizo.

Mazoezi hayo yanaonekana kama jaribio la utawala wa Rais wa Urusi Vladimir Putin kuonyesha nguvu za nyuklia na kuzizuia nchi za Magharibi ikiwemo Marekani, ambazo katika siku za hivi karibuni zimeipatia Ukraine idhini ya kushambulia maeneo lengwa nchini Urusi kwa kutumia silaha zilizotolewa na nchi hizo.