Hafla ya kuwakumbuka waathiriwa wa meli yafanyika nchini Japani

Raia wa Japani na Uturuki wametoa heshima zao kwa watu waliofariki wakati meli ya Uturuki ilipozama nje ya pwani ya mkoa wa Wakayama magharibi mwa Japani miaka 134 iliyopita.

Meli hiyo ya jeshi la majini iliyokuwa ikisafiri kwa jina Ertugrul ilizama nje ya Mji wa Kushimoto mnamo mwaka 1890. Watu zaidi ya 500 waliokuwa wameiabiri walifariki, lakini wakazi waliwaokoa watu wengine 69. Kisa hicho kinasemekana kusababisha uhusiano wa kirafiki kati ya nchi hizo mbili.

Hafla ya kumbukumbu ilifanyika jana Jumatatu mbele ya mnara wa kumbukumbu ya waliofariki wakati wa kisa hicho kwenye kilima unachoweza kuona eneo palipozama meli hiyo. Watu wapatao 130 waliweka maua kwenye mnara huo na kuomba kimyakimya.

Watu wengi upande wa Uturuki waliripotiwa kusafiri kwenye meli ya jeshi la majini ambayo ilikuja nchini Japani kuadhimisha miaka 100 ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya Japani na Uturuki.

Balozi wa Uturuki nchini Japani Korkut Gungen alisema amefurahi kwamba Kushimoto ni bandari ya kwanza kwa meli hiyo kutia nanga nchini Japani kwa sababu mji huo ni sehemu maalum kwa Uturuki. Balozi huyo pia alisema anatumai kwamba Uturuki na Japani zitaendelea kusaidiana.

Meya wa mji wa Kushimoto Tashima Katsumasa alisema atafanya kazi kwa bidii kudumisha historia ya urafiki ambayo imedumu kwa miaka 100.

Meli hiyo ya Uturuki itaondoka mjini Kushimoto leo Jumanne na itatembelea miji ya Tokyo na Hiroshima.