Japani na Marekani zafanya mkutano wa kwanza wa uendelezaji wa pamoja na uzalishaji wa vifaa vya ulinzi

Maafisa wa ulinzi kutoka Japani na Marekani walifanya mkutano wao wa kwanza juu ya uendelezaji wa pamoja na uzalishaji wa vifaa vya ulinzi.

Walikutana jijini Tokyo nchini Japani juzi Jumapili na jana Jumatatu. Waliohudhuria ni pamoja na Fukasawa Masaki ambaye ni Kamishna wa Idara ya Upataji, Teknolojia na Usafirishaji ya Wizara ya Ulinzi ya Japani, na mwenzake William LaPlante ambaye ni Naibu Kamishna wa Ulinzi wa Upataji na Uendelezaji kutoka Marekani.

Mkutano huo unafanyika baada ya Waziri Mkuu wa Japani Kishida Fumio na Rais wa Marekani Joe Biden kukubaliana mwezi Aprili kuanzisha jukwaa juu ya suala hilo.

Maafisa hao wamethibitisha kuwa watashirikiana kuimarisha sekta za ulinzi kwenye nchi zao kupitia uhamishaji wa teknolojia na njia zingine.

Pia wamekubaliana kuandaa makundi kazi manne ili kujadili uzalishaji wa pamoja wa vifaa, ikiwemo mifumo ya kudungua makombora ya PAC-3.

Kampuni zaidi ya 10 za Japani na Marekani zilishiriki kwenye mkutano huo wa jana Jumatatu. Washiriki walithibitisha kuwa serikali na sekta binafsi zitafanya mikutano.