Honda na Mazda zachunguzwa kuhusu jaribio la usalama wa magari

Timu ya wachunguzi kutoka Wizara ya Ardhi, Miundombinu, Usafirishaji na Utalii ya Japani imezuru katika ofisi za kampuni ya Honda Motor na Mazda Motor. Timu hiyo inachunguza kukiri kwa kampuni hizo kuwa zilifanya udanganyifu wa data za jaribio la usalama wa magari. Honda na Mazda ni kampuni za hivi karibuni kufanyiwa uchunguzi kati ya kampuni tano za utengenezaji magari baada ya kukiri kugushi majibu ya majaribio.

Timu ya wizara hiyo yenye maafisa watano ilifika makao makuu ya Honda jijini Tokyo leo Jumatatu.

Wizara hiyo inasema Honda ilifanya majaribio ya kelele isiyo ya kawaida katika aina 22 za magari ya zamani. Uzito wa magari hayo pia unasemekana kuzidi viwango vilivyotakiwa, ambavyo havikuonyeshwa kwenye ripoti za majaribio.

Kadhalika, wizara hiyo inasema kampuni hiyo ilighushi data za majaribio ya nguvu ya injini katika baadhi ya aina za magari.

Timu nyingine ya maafisa wanne waliwasili makao makuu ya Mazda mkoani Hiroshima leo mchana. Mazda imekiri kughushi majibu ya majaribio ya aina tano za magari, zikiwemo aina mbili ambazo bado zinatengenezwa.

Kwa aina hizo mbili za magari, kampuni hiyo kwa kudhamiria iliandika upya mfumo iliyoutumia kwa majaribio ya nguvu ya injini. Mazda imesimamisha utengenezaji wa aina hizo za magari.

Kampuni hiyo pia inasema haikufanya majaribio ya ajali ipasavyo kwa aina tatu za magari ambazo haitengenezi tena.