Korea Kusini yarusha matangazo ya vipaza sauti kuelekea Korea Kaskazini

Jana Jumapili, jeshi la Korea Kusini lilianza tena matangazo ya vipaza sauti vilivyoelekezwa Korea Kaskazini baada ya muda wa miaka 6. Hatua hiyo ni kukabiliana na mamia ya maputo ya taka ambayo Korea Kaskazini iliyatuma mpakani mwishoni mwa wiki hii.

Vyombo vya habari vya Korea Kusini viliripoti kuwa matangazo hayo ya jana Jumapili mchana yalijumuisha taarifa kadhaa za habari. Jeshi hilo linasema uendeleaji wa matangazo hayo utategemea kabisa na jinsi Korea Kaskazini itakavyojibu. Jeshi hilo linasema Korea Kaskazini inawajibika kikamilifu na mvutano ulioongezeka.

Korea Kusini imekuwa ikirusha matangazo ya habari, K-pop na ujumbe kuhusu haki za binadamu kwenye vipaza sauti karibu na eneo la mpaka wa kijeshi. Kampeni hiyo ilisitishwa baada ya mkutano wa viongozi wakuu baina ya nchi hizo mbili mnamo mwaka 2018.

Kim Yo Jong ni dada wa kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un. Alitoa taarifa kukosoa matangazo hayo ya jeshi la Korea Kusini.

Jana Jumapili, Wakuu wa Majeshi wa Korea Kusini walisema kuwa wamehesabu takribani maputo 330 tangu juzi Jumamosi usiku. Baadhi ya maputo yalipatikana katika mji mkuu, Seoul na Jimbo la Gyeonggi. Takribani maputo 80 yameripotiwa kutua ndani ya Korea Kusini.

Maafisa wa kijeshi wanasema maputo hayo yalikuwa yamebeba karatasi na takataka zingine lakini hadi sasa hakuna vitu vya hatari vilivyopatikana.

Korea Kaskazini inaonekana ilirusha maputo mengi zaidi kuelekea Korea Kusini jana Jumapili usiku.

Tukio hilo la hivi punde limetokea baada ya kundi la waasi wa Korea Kaskazini waishio Korea Kusini kutuma maputo yao siku ya Alhamisi wiki iliyopita. Maputo hayo yalikuwa yamebeba vipeperushi vya kumkosoa Kim Jong Un, pamoja na USB memory sticks zilizojaa tamthilia za Korea Kusini na taarifa zingine.