Shirika la haki za binadamu la UN: Raia wasiopungua 174 wameuawa nchini Ukraine mwezi Mei

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kufuatilia Haki za Kibinadamu nchini Ukraine linasema raia wasiopungua 174 wameuawa na 690 kujeruhiwa nchini Ukraine mwezi Mei.

Shirika hilo lilitangaza Ijumaa iliyopita kuwa hiyo ni idadi kubwa zaidi ya kila mwezi ya vifo vya raia tangu Juni 2023.

Aidha shirika hilo limesema idadi hiyo kubwa ya vifo imesababishwa na mashambulizi makali ya vikosi vya Urusi katika mji wa Kharkiv na kwingineko katika eneo la mashariki la Kharkiv baada ya Urusi kufanya mashambulizi nje ya mpaka wa kaskazini wa eneo hilo na Urusi mnamo Mei 10.

Jana Jumapili, vikosi vya Urusi vilifanya mashambulizi katika eneo la Kharkiv, na kuharibu nyumba maeneo hayo.

Katika video iliyotolewa juzi Jumamosi, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy alisema kwamba jeshi la Urusi limeshindwa kutekeleza operesheni yao katika eneo la Kharkiv.

Pia alisema vikosi vya Ukraine vinaviangamiza vikosi vya Urusi vinavyoingia katika eneo la Ukraine.