Mamlaka za Gaza: Operesheni ya kuokoa mateka wa Israel imeua Wapalestina 274

Mamlaka za afya katika Ukanda wa Gaza zinasema idadi ya Wapalestina waliouawa katika operesheni ya kijeshi ya Israel ya kuwaokoa mateka huko Nuseirat juzi Jumamosi imeongezeka hadi 274 huku 698 wakijeruhiwa.

Mateka wanne wa Israel waliokuwa wanashikiliwa na Hamas wameokolewa katika operesheni hiyo iliyofanyika katikati mwa Gaza ambayo ilianza saa tano asubuhi juzi Jumamosi wakati ambapo watu wengi walikuwa wakifanya manunuzi sokoni.

Jeshi la Israel limesema vikosi vyake vilipigana vikali kwa bunduki na wapiganaji wa Hamas wakati vikijaribu kuwaokoa mateka hao. Jeshi hilo limesema pia limefanya mashambulizi ya anga.

Kundi la kijeshi la Hamas limechapisha video siku hiyo hiyo, likidai kwamba mateka watatu waliohusika katika operesheni ya Israel wameuawa, na kuwa mmoja wao ni raia wa Marekani.

Jeshi la Israel limeendelea na mashambulizi ya anga na ardhini katika sehemu za katikati na kusini mwa Gaza jana Jumapili.

Mamlaka za afya katika ukanda huo zimetangaza kuwa idadi ya vifo imeongezeka hadi 37,084 tangu kuanza kwa mzozo wa sasa Oktoba mwaka jana.

Wakati huo huo, Waziri wa Ulinzi wa zamani wa Israel Benny Gantz jana Jumapili ametangaza kujiuzulu kutoka katika baraza la mawaziri la vita la nchi hiyo.

Gantz, mjumbe muhimu wa mrengo wa kati katika baraza hilo, mwezi uliopita alimtaka Netanyahu kuandaa mpango wa utawala ujao wa Ukanda wa Gaza. Pia aliashiria kuwa angejiuzulu kama Netanyahu hataandaa mpango huo kufikia juzi Jumamosi.

Katika mkutano na wanahabari, Gantz amemkosoa Netanyahu akisema, “uamuzi wa kimkakati wa mustakabali unatimizwa kwa kusitasita na kuchelewa kutokana na sababu za kisiasa.”

Ametoa wito wa kufanyika chaguzi mapema ili kupata imani ya watu.