Vyama vya mrengo mkali wa kulia vyatabiriwa kupata mafanikio katika chaguzi za bunge barani Ulaya

Utabiri wa awali uliotolewa na Bunge la Ulaya unaonyesha kuwa vyama vya mrengo wa kulia na mrengo mkali wa kulia vinatarajiwa kupata ushindi mnono katika chaguzi za Ulaya.

Upigaji kura kwa chaguzi hizo ulifanyika katika nchi 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya kuanzia Alhamisi iliyopita hadi jana Jumapili.

Nchini Ufaransa, chama cha mrengo mkali wa kulia cha National Rally kinatabiriwa kupata ushindi mnono dhidi ya muungano wa vyama tawala unaoongozwa na Rais Emmanuel Macron. Kinatarajiwa kupata viti zaidi ya mara mbili ya muungano wa Macron unaounga mkono Umoja wa Ulaya.

Chama hicho cha mrengo mkali wa kulia cha Ufaransa kinaupinga Umoja wa Ulaya kuendeleza msimamo wa Ulaya.

Kwa upande wake, Macron ametangaza kuvunja bunge la taifa na kuitisha chaguzi mpya, ambapo duru ya kwanza imepangwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu.

Katika hotuba kwa njia ya televisheni, Macron amesema kuongezeka kwa wafuasi wa utaifa na kile alichokiita wafitini ni hatari kwa Ufaransa na pia Ulaya.

Amesema ameamua kuwarejeshea wananchi uamuzi juu ya mustakabali wa Ufaransa kupitia kura.