Wanamageuzi wakubwa na wa wastani waondolewa kugombea urais nchini Iran

Serikali ya Iran imeweka wazi orodha ya watu sita walioruhusiwa kuwania uchaguzi wa urais Juni 28. Wagombea wengi ambao ni wanamageuzi wakubwa na wa wastani wameondolewa.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi hiyo jana Jumapili ilitangaza orodha ya wagombea wa uchaguzi huo, ulioitishwa baada Rais Ebrahim Raisi kufariki katika ajali ya helikopta mwezi uliopita.

Watu themanini walichukua fomu ya ugombea. Baraza la Ulinzi, au Jopo la wanasheria wa Kiislam, liliidhinisha watu sita tu kati yao kama wagombea baada ya kuchunguza sifa zao kama vile utiifu kwa mamlaka ya Kiislam ya nchi hiyo.

Watu hao sita wanajumuisha spika wa bunge Mohammad Baqer Qlibaf, ambaye aliwahi kuwa katika Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislam. Ni mtu mwenye msimamo mkali kama Raisi, ambaye utawala wake ulikuwa katika mvutano mkubwa na nchi za magharibi.

Orodha hiyo pia inajumuisha mhafidhina mwingine mwenye msimamo mkali, Saeed Jalili. Alikuwa katibu wa Baraza la Juu la Usalama wa Taifa, chombo kinachohusika na ulinzi wa taifa na masuala ya kigeni.

Mwingine aliyepenya katika ugombea ni Masoud Pezeshkian, aliyewahi kuwa naibu spika wa bunge na waziri wa afya. Ni mwanamageuzi anayetaka mazungumzo na nchi za magharibi.

Lakini wanamageuzi wengine wakubwa na wa wastani wameondolewa kwa sababu zisizojulikana.

Rais wa zamani Mahmoud Ahmadinejad, aliyekuwa maarufu miongoni mwa wanyonge, pia amezuiwa kugombea.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi hiyo imesema kampeni za uchaguzi zimeanza rasmi jana Jumapili.