Japani yaweka kikomo cha maombi ya hifadhi kupitia sheria iliyorekebishwa ya udhibiti wa uhamiaji

Japani inaanza kutekeleza sheria iliyorekebishwa ya Udhibiti wa Uhamiaji na Utambuzi wa Wakimbizi leo Jumatatu. Sheria hiyo itafanya raia wa kigeni ambao wameomba hifadhi ya ukimbizi mara tatu au zaidi kufukuzwa nchini Japani isipokuwa kama wana sababu zinazokubalika.

Mamlaka zinasema baadhi ya wageni wanajaribu kuepuka kufukuzwa nchini humo kwa kutumia vibaya mfumo ambao unasitisha zoezi hilo kwa muda wakati wa ushughulikiaji wa maombi yao ya hifadhi.

Sheria hiyo iliyorekebishwa pia inaruhusu wale wanaokabiliwa na ufukuzwaji kuishi chini ya usimamizi wa watu walioidhinishwa, badala ya kuishi kizuizini.

Idara ya Huduma za Uhamiaji inasema kuwa imeshuhudia uzuiwaji na uchunguzi wa muda mrefu wa watu wanaotafuta hifadhi ambao walikataa kuondoka Japani kurudi katika nchi zao.

Idara hiyo inaongeza kuwa hali hiyo ilifanya iwe vigumu kuwalinda kwa haraka wale ambao walihitaji ulinzi.

Hata hivyo, makundi yanayowasaidia wageni yanataja vikwazo katika sheria iliyorekebishwa, kama vile kushindwa kuhakikisha uwazi na usawa wa kutosha katika uchunguzi wa maombi ya hifadhi.

Wanasema sheria hiyo inaweza kuruhusu wanaotafuta hifadhi kurudishwa katika mataifa ambako wanaweza kuteswa.