Ukraine kukabiliwa na uhaba wa umeme msimu wa joto

Ukraine huenda ikakabiliwa na msimu mgumu wa joto kali kutokana na upungufu mkubwa wa umeme kufuatia mashambulizi ya Urusi kwenye vituo vya nishati kwa makombora na droni.

Waziri Mkuu wa Ukraine Denys Shmyhal aliviambia vyombo vya habari juzi Ijumaa kwamba ni asilimia 27 pekee ya mitambo ya nishati ya mvuke ya nchi hiyo iliyosalia katika mazingira sahihi ya utendaji kazi.

Mtendaji Mkuu wa shirika la nishati linaloendeshwa na nchi ya Ukraine, Ukrenergo alibainisha kwamba uharibifu kwenye mitambo ya umeme ni wa kiwango kikubwa zaidi mwaka huu kulinganisha na ilivyokuwa mwaka jana.

Vyombo vya habari vya eneo hilo viliripoti kwamba upungufu wa umeme utaongezeka zaidi katika msimu wa joto.

Taasisi ya Kimataifa ya Sosiolojia ya Kyiv, kampuni ya Ukraine ya utafiti wa maoni, ilitoa matokeo ya utafiti uliofanyika mwezi Mei ambapo, ilisema, kiwango cha uungwaji mkono kwa Rais Volodymyr Zelenskyy kilikuwa asilimi 59.

Ilisema mwezi Mei, 2022, muda mfupi baada ya kuanza kwa uvamizi wa Urusi, kiwango cha uungwaji mkono kwa rais huyo klilikuwa asilimia 90.

Kampuni hiyo ilisema raia wengi wa Ukraine wanaendelea kumwamini Zelenskyy lakini kiwango cha kumuunga mkono kinazidi kupungua.

Ilisema sababu kuu ni kwamba watu wanahisi mzigo wa vita si wa haki na kwamba kupambana na ufisadi bado hakujaendelea kiasi cha kutosha.

Rais Vladimir Putin wa Urusi alidai katika hotuba yake juzi Ijumaa kwamba Zelenskyy amepoteza uhalali baada ya uchaguzi wa urais uliopangwa kufanyika mwezi Machi kutofanyika.

Urusi imekuwa na ina nia ya kuharibu uaminifu wa Zelenskyy miongoni mwa raia wa Ukraine, ikitumai kwamba itapelekea katika mabadiliko ya utawala.