Korea Kaskazini yatuma tena maputo yenye taka nchini Korea Kusini

Jeshi la Korea Kusini limesema Korea Kaskazini imetuma tena maputo yenye taka nchini Korea Kusini ikiwa ni jibizo la dhahiri la harakati za kusambaza vipeperushi vya kuipinga Korea Kaskazini za kikundi kimoja cha wanaharakati nchini Korea Kusini.

Mnadhimu Mkuu wa Jeshi alisema hadi kufikia saa tano usiku jana Jumamosi, maputo hayo yalisafiri upande wa mashariki kutoka kaskazini mwa jimbo la Gyeonggi karibu na mji mkuu Seoul na huenda yalipelekwa na upepo upande wa kusini.

Ni mara ya tatu tangu mwezi Mei ambapo Korea Kaskazini inatuma idadi kubwa ya maputo yenye taka nchini Korea Kusini.

Juni 2, naibu waziri wa ulinzi wa Korea Kaskazini alitangaza kusitisha kwa muda operesheni maputo.

Afisa huyo alisema operesheni hiyo itaendelea ikiwa vipeperushi vya kuipinga Korea Kaskazini vitatumwa nchini humo na Korea Kusini.

Aliongeza kuwa nchi hiyo itajibu kwa kutuma maputo yenye taka mara 100 zaidi ya ujazo wa vipeperushi vya propaganda.

Tukio la hivi karibuni limekuja baada ya kikundi kimoja cha waliokimbia nchini Korea Kaskazini na kuingia Korea Kusini Alhamisi wiki hii kutuma maputo yenye vipeperushi vinavyomkosoa kiongozi mkuu wa Korea Kaskazini Kim Jong Un, sambamba na USB zenye ngoma na data zingine za Korea Kusini.

Serikali ya Korea Kusini inafikiria kurejesha matangazo ya propaganda ya kutumia spika iliyoelekezwa Korea Kaskazini karibu na mpaka wa kijeshi unaotenganisha mataifa hayo mawili ya Korea.