Macron, Biden wathibitisha tena mshikamano kuisaidia Ukraine

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesisitizia mshikamano wa nchi yake na mataifa mengine ya Magharibi katika kuisaidia Ukraine.

Macron amefanya mazungumzo na Rais wa Marekani Joe Biden jijini Paris jana Jumamosi, siku moja baada ya kukutana na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy.

Katika mkutano wa pamoja na wanahabari, Macron alisema kuwa Ufaransa, Marekani na mataifa mengine ya Magharibi lazima yaendelee kutoa msaada kwa Ukraine ili kulinda usalama na uthabiti wa Ulaya.

Rais huyo wa Ufaransa aligusia kuwa kwa kipindi cha miezi michache iliyopita, mataifa ya Magharibi yameidhinisha Ukraine kushambulia malengo ndani ya eneo la Urusi kwa kutumia silaha zilizotolewa na mataifa ya Magharibi na kupanga kuunda muungano wa mataifa ambayo yatapeleka wakufunzi wa kijeshi ili kutoa mafunzo kwa vikosi vya Ukraine.

Macron alielezea matumaini kuwa viongozi wa Kundi la Nchi Saba zilizoendelea zaidi kiviwanda duniani, G7 pia yatajidhatiti katika kusaidia Ukraine pale yatakapokutana katika mkutano wa viongozi wakuu utakaoanza Juni 13 nchini Italia.

Biden alisema: “Putin hatoishia Ukraine. Si tu Ukraine. Ni zaidi ya Ukraine. Bara la Ulaya lote litatishiwa.”

Aliongeza kuwa, “Marekani ipo imara na Ukraine. Tunasimama na washirika wetu.”