Mchezaji tenisi wa Japani Oda ashinda taji lake la pili la michuano ya Wazi ya Ufaransa ya viti vya magurudumu

Mchezaji nyota wa tenisi wa Japani Oda Tokito ameshinda kwa mara ya pili mfululizo katika Michuano ya Wazi ya Ufaransa kwa upande wa wanaume ya viti vya magurudumu, na taji lake la nne la michuano mikubwa.

Katika mchezo wa fainali wa mashindano hayo jijini Paris jana Jumamosi, Oda mwenye umri wa miaka 18, anayeshika nafasi ya pili kwa ubora duniani, alimshinda Gustavo Fernandez wa Argentina, anayeshikilia nafasi ya tatu kwa ubora duniani kwa 7-5, 6-3.

Mwaka jana, akiwa na umri wa miaka 17 na mwezi mmoja, Oda alishinda taji la Michuano ya Wazi ya Ufaransa, na kuwa mshindi wa kwanza mwenye umri mdogo zaidi wa taji kubwa katika kipengele hicho.

Pia alishinda fainali ya wanaume ya Wimbledon mwaka jana kwa mchezaji mmoja mmoja, na Mashindano ya Wazi ya Australia mapema mwaka huu.

Fainali ya jana Jumamosi ilifanyika kwenye uwanja wa Roland Garros, itakapofanyika Mashindano ya Paralimpiki ya Paris yatakayoanza baadaye mwezi Agosti mwaka huu.

Oda anatarajiwa kuiwakilisha Japani kwenye Paralimpiki.